Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mheshimiwa Amina Makilagi, amesema Ushirika wa Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) ukitumiwa na kuongozwa vizuri ni mkombozi wa uchumi kwa wanawake nchini.

Mhe. Makiagi amesema kupitia SACCOS mwanamke anaweza kufanya mambo mengi ya maendeleo kama atatumia mfumo mzuri wa kukopa na kurejesha. Ameeleza hayo leo tarehe 22/10/2023 wakati wa Kongamano la Jukwaa la Wanawake wa SACCOS Kitaifa lililofanyika Jijini Mwanza.

Vile vile ametoa rai kwa wanawake kwenye SACCOS kuchangamkia fursa za kibiashara zinazotangazwa Serikalini kuomba na kuzifanya ili kuendelea kukuza mitaji katika Vyama vyao.

“Tenda za Serikali ni kwaajili ya watu wote, wanawake kwenye SACCOSS changamkieni hizo fursa kwa kujiingiza katika biashara ili mitaji yenu iwe mikubwa muweze kukopa fedha nyingi kwa ajili ya kufanya mambo ya kimaendeleo," amesema.

Naye Mwenyekiti wa Kongamano hilo, Somoe  Nguhwe, amesema wanaendelela kuhakikisha wanawake wanagombea nafasi za uongozi katika SACCOS zao.

Nguhwe ameeleza kuwa na SACCOS zinaongozwa na wanawake ndiyo ambazo zinaongoza kwa Hati Safi hii inaoesha wanawake wanafanya kazi nzuri na wanaweza zifikisha mbali SACCOS hizo.