Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Dkt. Benson Ndiege, amekipongeza Chama Kikuu cha Ushirika cha Wilaya za Ruangwa, Nachingwea na Liwale RUNALI LTD kwa  kujenga Kiwanda cha kukamua mafuta chenye Thamani ya Shilingi 143,816,000 ambacho kitaongeza  thamani  ya mazao ya wanachama wao pamoja na wakulima kwa ujumla kwa kutumia mapato ya ndani.

Amesema hayo tarehe 07 Desemba, 2023 wakati akifungua Kiwanda hicho ambapo  ameeleza kupitia mradi huu wa kiwanda hicho Chama kitaenda kuongeza thamani ya mazao ya wakulima ambayo hapo awali yalikuwa yanauzwa yakiwa ghafi.

“Sasa niwaombe watendaji na wasimamizi watakaoajiriwa katika kiwanda hiki kufanya kazi kwa ufanisi naweledi ili kiwanda hiki kiweze kuwa na tija kwa wakulima wetu maana hii ni fedha ya wakulima wetu,” amesema Dkt. Ndiege.

Pia amewapongeza RUNALI namna ambavyo wameendelea kutekeleza majukumu yao kwa kusimamia malipo ya wakulima kwa wakati hasa katika vipindi vya mauzo ya mazao katika kipindi cha miaka ya karibuni na Tume ya Maendeleo ya Ushirika imeshuhudia kupungua  kwa migogoro hasa kipindi cha misimu ya mauzo ya mazao.

"Hii inaonesha kuwa usimamizi pamoja na weledi kwenye Vyama vya Ushirika unaendelea kuimarika zaidi," amesema Mrajis.

Naye Afisa Masoko wa RUNALI, Beatrice Liungulu, amesema mradi huu unatarajia kunufaisha wakulima zaidi ya 30,000 wanaohudumiwa na Chama cha RUNALI kwa kuongeza kipato kupitia zao la Alizeti hivyo kuendelea kuhamasisha kilimo cha Alizeti kwasababu linaweza kulimwa na mazao mengine kwenye shamba moja.

Pia Beatrice amesema kupitia Mradi huo Kiwanda kitazalisha mafuta halısı ya kupikia yanayotokana na mbegu mbalimbali ikiwemo Alizeti, Ufuta, Karanga na Mbegu za Maboga ambayo yatapatikana kwenye ujazo wa lita tano, lita tatu lita moja na nusu lita.