Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Elikana Balandya ametoa wito kwa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) kujiunga na Muungano wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo Tanzania (SCCULT) ili kuwa na uwakilishi wenye nguvu ambao upo imara na wenye kujiletea maendeleo.
Ametoa wito huo leo tarehe 26 Oktoba, 2023 wakati wa kilele cha Maadhimisho ya wiki ya Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo yaliyofanyika Mkoani Mwanza.
Amesema kuwa viongozi wa SACCOS waendelee kutangaza masuala mazuri ambayo Ushirika wa Akiba na Mikopo umefanya kwa wanachama wake na shuhuda za kuaminika ndiyo utakuwa sehemu ya uhamasishaji ambao utaleta picha na mwonekano mzuri wa Ushirika wa Akiba na Mikopo.
Pia ameeleza ili SACCOS zizizidi kuwa imara na zenye muelekeo mzuri wanachama wanapaswa kukopa na kulipa kwa wakati ili kuvipa nguvu vyama vyao na kuwapa wanachama wengine nafasi ya kupata huduma ya mikopo.
Akizungumza katika Maadhimisho hayo, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Dkt. Abdulmajid Nsekela, amesema kuendelea kuboresha SACCOS kutachangia kwa sehemu kubwa maendeleo na uchumi wa nchi. Hivyo, amewataka viongozi na wanachama waendele kuungana katika kuimarisha usimamizi wa shughuli za Vyama vyao.
Kwa upande wake Mrajis na Mtendaji wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Dkt. Benson Ndiege, amesema kupitia SACCOS watu wamepata ajira 13,677 za kudumu na za muda mwaka 2022 ikilinganishwa na ajira 13,496 zilizokuwepo mwaka 2021. Aidha, SACCOS zimeendelea kujali jamii kwa kutoa huduma mbalimbali za kijamii kwa kuzingatia msingi wa 7 ambapo mwaka 2022 jumla ya watanzania 438,409 walipata Msaada kutoka kwenye SACCOS yenye thamani ya Shillingi Milioni 635.38.