Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, ametoa wito kwa AMCOS zote nchini kuingia katika mpango maalum wa kukata Bima ya mazao ili kuweza kulinda mtaji.
Mrajis ameyasema hayo leo Machi 26, 2024 wakati akifungua Mkutano wa sita wa Chama Kikuu cha Ushirika Milambo unaofanyika kwa muda wa siku mbili kuanzia Machi 26 hadi 27, 2024 wilayani Urambo mkoani Tabora.
"Natoa wito kwa AMCOS zote kuingia katika mpango maalum wa kukata bima ya mazao ili kuweza kulinda mtaji; tunafahamu kwamba msimu wa kilimo wa mwaka 2022/2023 baadhi ya wanachama walipata majanga ya mvua ya mawe, kuanguka mabani na kuungua kwa tumbaku na hivyo kurudisha nyuma maendeleo ya mkulima na chama na kushindwa kufikia malengo," amesema Mrajis.
Awali kabla ya ufunguzi wa mkutano huo, Mrajis alifungua ofisi za Chama Kikuu cha Ushirika Milambo, na kuzindua pikipiki nne (4) zitakazotumika na maafisa ugani na uzinduzi wa gari la chama na kushiriki zoezi la upandaji miti ikiwa ni sehemu ya kutimiza msingi wa saba wa Ushirika wa kuijali jamii.
Aidha, Mrajis amesisitiza kuhusu matumizi ya Mfumo wa kidigitali wa Vyama vya Ushirika (MUVU) ambapo ameelekeza wanachama wa AMCOS na wakulima wote wawe wamesajiliwa katika mfumo huo kabla ya tarehe 31/03/2024.
Dkt. Ndiege ametoa rai kwa Vyama vyote kununua hisa ili kujenga mtaji imara wa Benki ya Taifa ya Ushirika ili iweze kutoa mikopo kwa wanaushirika na wananchi wengine kwa riba ya ushindani ukilinganisha na benki nyingine.