Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania(TCDC), Dkt. Benson Ndiege,   ametoa onyo kwa viongozi wa Vyama vya Ushirika ambao bado wanaishi katika uongozi wa kijanja kijanja na kuacha kufuata miongozo na kanuni za Ushirika.

Amesema  hayo leo tarehe 11 Novemba, 2023 wakati wa kongamano la Vyama vya Ushirika Wilaya ya Songwe  akimwakilisha Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussen Bashe, na kueleza kuwa Viongozi ambao watafanya kazi  nzuri TCDC itawaunga mkono, na mbaye atavuruga, Tume haitaweza kumvumilia; hivyo,
amewataka kuendelea kufanya kazi kwa weledi na   kusimamia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala.

Vilevile amewataka wakulima wa Songwe kuendelea kujiunga katika Vyama vya Ushirika kwenye maeneo yao ili waweze kuwa na sauti ya umoja ambayo italeta maendeleo katika Vyama.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Mhe. Solomon Itunda, amesema kwa kutumia kwao Mfumo wa Stakabadhi za Ghala katika zao la Ufuta, kumesabababisha ongezeko la mapato katika Wilaya hiyo kutoka kukusanya Millioni 300 kwa mazao yote na kufikia millioni 800 kwa zao la Ufuta tu.

Amesema mafanikio hayo si kwa Halmashauri tu hata kwa mtu mmoja mmoja wameweza kujipatia fedha nzuri kutokana na kuuza kwa kufuata Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwani wananchi wamepata mwitikio wa kuuza mazao yao kwa kufuata utaratibu.

Naye Kaimu Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika Songwe (SORECO),  Mon Mwampamba,  amesema kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala
 kumekuwa na ongezeko la ubora  wa Ufuta  na kupelekea ongezeko la bei za Ufuta kutoka Shilingi 1,700 ya awali hadi kufikia Shilingi 3,847  kwa kilo moja ya Ufuta hali hii imepelekea wananchi kuachana na uuzaji holela wa Ufuta.