Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, ameteua Wajumbe wa Bodi ya Mpito ya Shirikisho la Vyama Vya Ushirika Tanzania Bara (TFC)  kwa mamlaka aliyonayo chini ya Sheria ya Vyama vya Ushirika Na.6 ya mwaka 2013.

Wajumbe walioteuliwa ni: Tito Haule (Mhadhiri, Taasisi ya Uhasibu Tanzania - TIA), atakuwa Mwenyekiti; Prof. Isaack Kazungu (Mhadhiri, Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi - MoCU); Wakili Shani Mayosa (Mkurugenzi, Huduma za Sheria - TIC); Tuse Joune (Mkurugenzi Mtendaji, Tanzania Bankers Association); Justica Masinde (Makamu Mwenyekiti, Bandarini SACCOS Ltd);
Meja Michael Moyo (Mjumbe, Bodi ya Ngome SACCOS Ltd); Karimu Chipola (Mwenyekiti, Chama Kikuu cha Ushirika Tandahimba na Newala -TANECU Ltd); Shedrack Issangya (Mwenyekiti, Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Arusha); na  Eliwaza Mkilya (Mjumbe, Bodi ya Mwenge Housing Cooperative Society Ltd).

Dkt. Ndiege amesema uteuzi huo umezingatia elimu, weledi, uzoefu, jinsia, na kaliba za wahusika; ikiwemo watu wa kutaka matokeo chanya ambao wanaweza kuifikisha TFC kwenye Maendeleo yanayohitajika.

Mrajis ameitaka Bodi hiyo ya Mpito baada ya makabidhiano na Bodi iliyomaliza muda wake kufanya tathmini ya Watendaji waliopo TFC kama wanaleta tija kwa Shirikisho, na utendaji wao unakidhi mahitaji na malengo ya Shirikisho ya wakati uliopo.

Aidha, Dkt. Ndiege amesema Ofisi ya Mrajis ipo tayari kushirikiana na Bodi ya TFC kutafuta Mtendaji Mkuu wa Shirikisho kama ilivyofanya katika Vyama Vikuu vya NCU LTD, SIMCU LTD na  KNCU LTD.

Pia ameelekeza Bodi mpya kufanyia kazi Hoja za Mkaguzi wa Nje (COASCO) na Kuweka Mkakati thabiti wa kusimamia Shirikisho kwa Kuandaa Mpango Mkakati utakaoendana na wakati wa sasa, utakaotumika kama malengo mahsusi ya Shirikisho.