Mrajis na Mtendaji Mkuu Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) ameeleza kuwa Suala la Vyama vya Ushirika wa Kilimo kuwa na mashamba ndiyo mwelekeo wa Ushirika nchini ambao unataka Vyama kuwa na Mashamba ya mfano ambayo yatamilikiwa na Vyama.
Hayo yameelezwa na Dkt. Ndiege walipotembelea shamba la Chama Kikuu cha Ushirika Masasi (MAMCU) leo tarehe 3/03/2024 ambapo aliambatana na Mkurugenzi Mkuu wa COPRA ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamisheni ya TCDC, Irene Madeje, Mkurugenzi wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Asangye Bangu na Mkurugenzi wa Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), Godfrey Malekano wametembelea shamba la Chama Kikuu cha Ushirika MAMCU.
Dkt Ndiege amesema Vyama vikimiliki mashamba makubwa kama la MAMCU itasaidia kupunguza makato kutoka kwa wanachama ila pia itarahisisha upatikanaji wa mbegu hali itakayopelekea kumpunguzia mwanachama gharama za uzalishaji wakati wa kupanda.
“Tukiendelea hivi tunaimani baada ya muda wanachama wetu watapata huduma bure katika Vyama vyao kwasababu Vyama vitakuwa vimesimama kiuchumi na ndiyo tunataka Ushirika wa namna hiyo wa kujiendesha bila kutegemea michango ya wanachama,” amesema Dkt Ndiege
Naye Mkurugenzi Mkuu COPRA ametoa Pongezi kwa Chama cha MAMCU kwa kuonesha uthubutu wa kuanzisha shamba hilo ambalo limeshapandwa na kuahidi Mamlaka yake itashirikiana katika kusimamia upandaji wa kisasa na kutafuta soko la mazao hayo ambayo taasisi ya COPRA yanayasimamia.
Kwa upande wake Meneja Mkuu MAMCU, Biadia Matipa, amesema shamba hilo la kimkakati la hekari 500 wamefanikiwa kupanda ufuta hekari 200 na mbaazi hekari 300 ambazo zimepandwa kwa kufuata utaratibu na mategemeo mpaka 2025 watakuwa wamelima hekari 700.
Wakati huo huo viongozi hao wamefanya kikao na Viongozi wa Vyama Vikuu vya Ushirika vya TAMCU na SONAMCU Wilayani Tunduru.