Makamishna wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), wamefanya ziara ya kutembelea vitega uchumi vya Chama Kikuu cha Ushirika Nyanza (NCU) ikiwemo Majengo na Hosteli zilizopo katikati ya Jiji la Mwanza na eneo la KAUMA kwenye jengo na ghala la kukodi pamoja na kituo cha mafuta.

Vilevile, Makamishna wametembelea kiwanda  cha kuchambua Pamba kilichopo eneo la Manawa wilayani Misungwi.

"Hiki kiwanda cha kuchambua Pamba kiliundwa mwaka 1990 na kilichangia sana maendeleo ya zao la Pamba kwani mikoa 7 ya Kanda hii ya Ziwa na jirani ilikuwa inaleta Pamba na kuchambuliwa kabla ya kukifunga mwaka 2014; tumeomba fedha Serikalini Shilingi milioni 800 ili tuweze kukifufua," amesema Elisha Midamo, Meneja Uzalishaji wa NCU.

Kamishna Richard Mayongela amekishauri chama hicho kukutana na uongozi wa Benki mbalimbali ili uweze kupata mkopo wenye riba nafuu kupitia mali ilizonazo zenye thamani kubwa.

"Ziara yetu ya siku mbili tukiwa hapa Mwanza tutahimiza sana chama hiki kiwe na wingi wa wanachama wake ambao ndiyo mtaji wa kuwa na nguvu pia kitumie vizuri fursa za mali zake kujiongezea kipato," amesema Mayongela.

Ujumbe huo utamaliza ziara yake leo Novemba 28, 2023 kwa kuzitembelea baadhi ya Saccoss zilizopo Wilaya za Nyamagana,Ilemela na Magu.