Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeviagiza Vyama vya Ushirika nchini kuwasaidia wanachama wao na sio kuwa mzigo kwa wanachama ikiwemo kukomesha ubadhilifu katika Vyama hivyo.

Agizo hilo limetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mhe. Mariam Ditopile, wakati wa kupokea Taarifa ya Maendeleo ya Uanzishwaji wa Benki ya Ushirika Tanzania katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo na Viongozi wa Ushirika.

Mheshimiwa Ditopile amesema wanaushirika nchini wanahitaji kuwezeshwa ili waweze kukua kiuchumi na kujisimamia katika shughuli zao hivyo kupitia Benki ya Ushirika wanachama wa Ushirika watanufaika.

“Benki hii ikisimamia misingi ya kiutendaji, Vyama vya Ushirika vitanufaika kwani wataweza kupata mikopo ambayo itawasaidia katika kuendesha shughuli zao na tunategemea benki hii ifanye vizuri kama benki  za ushirika katika nchi nyingine,” amesema Mhe. Ditopile

Naye Mrajis na Mtendaji Mkuu Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege, ameeleza kuwa viongozi na watendaji ambao wamefanya ubadhilifu na kuchafua taswira ya Ushirika wanachukuliwa hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa viongozi wengine.

“Hatuwezi kurudi kwenye Ushirika wa zamani wa kulalamikiwa kwani sasa hata viongozi wapya wanaochaguliwa wanafanyiwa upekuzi na mamlaka mbalimbali ili kuhakikisha hatupati viongozi ambao watakuja kuvuruga mwenendo mzuri tunaoenda nao sasa wanaushirika,” amesema Dkt. Ndiege.

Naye Meneja Mkuu wa Benki ya Ushirika Kilimanjaro (KCBL), Godfrey, Ng'ura, amesema ushirika ni sekta mtambuka na wakati wake wa kuwa na benki ya ushirika ili iweze Kupanua wigo wa njia za mapato na tija kwa Vyama vya Ushirika na wakulima wadogo na kupata gawio katika benki  tarajiwa ya ushirika

Pia ameeleza benki hii italeta ujumuishi wa kifedha na makundi ya wakulima na wajasiriamali walio nje ya mfumo wa fedha, pia kutakuwa na fursa za kibiashara ndani na nje ya sekta na masoko endelevu na sekta ya ushirika nchini.