Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Mhe. Dunstan Kyobya, ameipongeza Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) katika kusimamia kusimamia Maendeleo ya Ushirika Nchini na  ametoa rai kwa Tume kuendelea kuhamasisha na kuanzisha Vyama vya Ushirika katika maeneo yote ya wilaya ya Kilombero ambayo hayana Vyama vya Ushirika ili kuweza kuwanufaisha wananchi kukuza uchumi wao.

Mhe. Kyobya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kikao cha Baraza la Biashara la Wilaya ametoa rai hiyo leo Februari 20, 2024 alipokuwa akifunga Kikao cha Baraza la Biashara cha Wilaya hiyo kilichofanyika mjini Ifakara, Wilayani Kilombero.

"Nikuombe Naibu Mrajis wa TCDC na wadau wengine, WRRB na TMX mje kwenye maeneo yetu kuanzisha Vyama vya Ushirika ili wananchi wetu wanufaike kupitia Ushirika," amesema Mhe. Kyobya.

Akimwakilisha Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Naibu Mrajis (Uhamasishaji) Consolata Kiluma, amewasisitiza wananchi kujiunga na Vyama vya Ushirika na kutaja mambo makuu mawili yanayofanywa na TCDC kupitia Uhamasishaji na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika.

"TCDC tuna majukumu makuu mawili; jukumu la kwanza ni uhamasishaji na uanzishwaji wa Vyama vya Ushirika na jukumu la pili ni Usimamizi wa Vyama vya Ushirika nchini, hivyo katika kutekeleza Majukumu haya tunawasisitiza wananchi kujiunga na Vyama vya Ushirika ili kuweza kupata faida zilizomo kwenye Ushirika ikiwemo kuwezeshwa kupata mitaji," amesema Naibu  Mrajis.

Katika kikao hicho wadau wa Ushirika; Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala ( WRRB) waliwasilisha mada kuhusu "Mfumo wa Stakabadhi Ghala" na kwa upande wa Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) waliwasilisha mada kuhusu "Mfumo wa Soko la Bidhaa Tanzania".

Kikao hicho kilihudhuriwa na Wakuu wa Taasisi mbalimbali, Watendaji wa Kata, Wakuu wa Idara na Kamati ya Usalama.