Mrajis na Mtendaji Mkuu Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, amezindua miradi ya Shilingi 899,123,987 iliyotekelezwa kwa fedha za ruzuku ya jamii zilizotokana na mauzo ya Kahawa Maalum kwa msimu wa mwaka 2022/2023 katika Chama Kikuu cha Ushirika cha Karagwe (KDCU).
Dkt. Ndiege amezindua na kugawa vitendea kazi ikiwa ni pamoja na Pikipiki 23 zilizogharimu Shilingi 64,400,000, Vishikwambi 40 vyenye thamani ya shilingi 37,600,000, Ununuzi wa mashuka 500 kwa ajili ya wodi ya kina mama iliyoghalimu Shilingi 11,720,650, Mtaji anzia wa SACCOS 150,000,000 na Mgao wa Vyama vya Msingi kwa ajili ya kuboresha miundo mbinu kwa kiasi cha shilingi 225,000,000.
Dkt. Ndiege amefanya uzinduzi huo leo tarehe 24 Novemba, 2023 Mjini Karagwe, ikiwemo kuzindua wa Mradi wa ujenzi wa uzio na bweni kwa Shule ya Sekondari Nyaishozi inayomilikiwa na Chama Kikuu Ushirika cha Karagwe KDCU utakaogharimu shilingi million 700 na mradi wa Kisima cha Maji katika ofisi ya KDCU ulioghalimu Shilingi millioni 13.
Dkt. Ndiege amesema, Vyama vyote vya Ushirika vinapaswa kufanya mambo ya kuwanufaisha wanachama wake kama ambavyo KDCU imeweza kufanya kwani chama ni mali ya wanachama na wao ndiyo wanapaswa kunufaika zaidi.
Kwa upande wake Kaimu Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika, Domitiani Robert amesema KDCU inamatarajio ya kuongeza AMCOS nyingine katika Mradi wa Kahawa Maalum ili kujenga uzalishaji endelevu na wenye tija kwa wakulima na pia ameeleza kuwa Chama kitaajiri Maafisa Ugani ili kukidhi matakwa ya mradi huo.