Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, ametoa rai kwa Bodi mpya ya  Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Pwani (CORECU - 1984 LTD) kufanya kazi kwa kusimamia misingi ya Ushirika na kwa maslahi ya wanachama wao.

Amesema hayo  leo tarehe 30/04/2024 wakati wa Mkutano Mkuu wa 30 wa Chama hicho uliofanyika mjini Kibaha ambapo uliambatana na Uchaguzi wa Bodi chama hicho.

Mheshimiwa Kunenge amesema Viongozi waliochaguliwa wanatakiwa kufanya kazi kwa malengo ili waweze kukisogeza Chama hicho mbele na si kukirudisha nyuma kwani CORECU ilipofika sasa inapaswa kuimarishwa zaidi ili iendelee kufanya vizuri.

“Mimi nataka kufanya kazi na viongozi wanaofanya kazi kwa maslahi ya wananchi na ambao wanasimamia chama kızıdi kufanya vizuri kama umechaguliwa katika bodi na ni mjumbe mpya ujue kabisa sivumili watu wazembe nataka tufanye kazi kwa bidii ili Ushirika uzidi kuwa na manufaa kwa Wananchi,” amesema Mheshimiwa Kunenge.

Wakati huo huo Wanachama Cha Chama cha Ushirika Mkoa wa Pwani wamemchagua Musa Mng’esele  kuwa Mwenyekiti wa Chama hicho na Bodi ya Wajumbe sita ambao ni Josephat Mwambega, Mussa Pazi, Dollah Chaurembo, Hadija Omari, Burton Nsape, Mussa Mngeresa na Mwakilishi Kassim Mpeluye ambao wamechaguliwa na wanachama wa Chama hicho.

Katika mkutano huo, Vyama vya Ushirika Mkoa wa Pwani wamekabidhi  Misaada kwa Mhe. Kunenge kwa ajili ya waathirika wa mafuriko katika Wilaya za Rufiji na Kibiti ambayo ni Mchele Tani nne na maharage nusu Tani.