Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Afrika inahitaji kurejesha hadhi yake kwenye tasnia ya Kahawa Duniani.
Mhe. Rais Dkt. Samia amepongeza nchi za Afrika kuja pamoja kujadili uendelezaji wa zao hilo na Umoja wa Afrika kuliingizia zao la Kahawa kwenye mazao ya kimkakati hatua ambazo ni muhimu katika kuanza kurejesha hadhi ya Afika kwenye tasnia ya Kahawa duniani.
Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo Februari 22, 2025 katika Mkutano wa Tatu wa nchi 25 wazalishaji wa Kahawa Barani Afrika uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es salaam.
Rais Dkt. Samia amesema, licha ya tasnia ya Kahawa kukabiliwa na changamoto anuai, Bara la Afrika limeanza kupiga hatua katika kukabiliana na changamoto hizo. Aidha, ameeleza imani yake ya kuwa na jukwaa hilo la nchi wazalishaji wa Kahawa Barani Afrika litaweza kuunganisha nguvu katika kukabiliana na changamoto zinazoikumba Sekta ya Kahawa Barani Afrika na kuwa nyenzo sahihi ya kufikia malengo waliyojiwekea.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Samia amezitaka nchi za Afrika ziazimie kuwa ifikapo 2035 nusu ya Kahawa inayozalishwa Barani Afrika iongezewe thamani Barani Afrika kabla ya kuuzwa ndani na nje ya bara hilo.
Akifafanua kuhusu manufaa ya zao la kahawa, Rais Dkt. Samia amesema takwimu zinaonesha kuwa manufaa zaidi ya zao hilo yapo kwenye mnyororo wa thamani mzima kuliko uzalishaji. Hivyo, Afrika inahitaji kuwa na viwanda vingi zaidi vya kuchakata Kahawa na vya kutengeneza bidhaa nyingine zinazotokana na mabaki ya zao hili.
Rais Dkt. Samia amesema kuendelea kusafirisha Kahawa ghafi ni kuendelea kusafirisha ajira za vijana zinazohitajika Afrika, kujikosesha mapato zaidi ambayo yanahitajika kwa maendeleo ya Bara la Afrika na kumfanya mkulima wa Kahawa aendelee kukosa soko la uhakika wa anachokizalisha.