Mrajis wa Vyama Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Dkt. Benson Ndiege, amezitaka Bodi na Menejimenti  za Vyama Vya Ushirika kuhakikisha mizani zote zimekaguliwa na Wakala wa Vipimo.

Amesema ni wajibu wao kuhakikisha kila Mwendesha Ghala anatumia mizani iliyokaguliwa kwa lengo la kufanya kazi kwa kufuata sheria na taratibu na pia kutumia kifaa ambacho hakiwezi kupunja haki ya mkulima.Mrajis ametoa wito huo leo tarehe 17/11/2022 wakati wa ufunguzi wa ghala la Namitili AMCOS,  Tunduru na amewataka wakulima kuendelea kutumia Mfumo wa Stakabadhi Ghalani ambao unasaidia katika ushindani wa bei kwa wanunuzi na hivyo wakulima kunufaika.

Pia ameagiza viongozi wa AMCOS kuhakikisha kila mwanachama na mkulima anafungua akaunti ya benki ili malipo yao ya fedha yapokelewe kwa njia ya benki. “Hizi si zama za kulipana fedha taslimu, kila mkulima afungue akaunti na pia itasaidia kuepusha utapeli, wizi na uporaji hivyo viongozi wa AMCOS na Maafisa Ushirika mhakikishe hakuna mtu analipwa fedha taslimu. Nimefurahi Wanatunduru leo mmekubali kuuza Korosho zenu kwa bei ya 1890," amesema Mrajis.

Dkt. Ndiege amewapongeza watu wa Ruvuma kwa namna wanavyojipambanua na kulima mazao tofauti tofauti kama Soya na Tumbaku ambayo kwa Kusini maeneo machache wanalima mazao hayo. “Mnafanya vizuri sana wakulima wa Ruvuma na ndiyo maana Mkoa wenu upo nafasi ya tatu kitaifa kwa uzalishaji wa zao la korosho kwa wingi na katika Mkoa wa Ruvuma Wilaya ya Tunduru  ndiyo imekuwa kinara wa uzalishaji wa zao la korosho misimu yote” amesema Dkt. Ndiege.

Naye Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru (TAMCU LTD), Mussa Manjaule alieleza  Chama Kikuu wamekuwa na mipango ya kujenga kiwanda cha kubangua Korosho na Ujenzi wa ofisi ya chama ambayo itakuwa ya ghorofa.Amesema Mipango hii itafanikiwa na wataendelea kufanya mambo ya maendeleo kwasababu ya kutumia mfumo wa Stakabadhi Ghalani wanaotumia katika kuuza mazao ya wakulima hususan Korosho, Ufuta na Mbaazi.

Mwenyekiti Manjaule wa TAMCU LTD amemuomba Mrajis kufuta wadai na wadaiwa wa Chama Kikuu walioko kwenye hesabu ya chama kama ambavyo mkutano Mkuu uliazimia kuomba kufutwa madeni hayo.

Aidha, Mwenyekiti huyo alieleza kuwa kumekuwa na tabia ya wanunuzi kuwashawishi wakulima kutokupeleka mazao ghalani hususani mbaazi hivyo wanaomba Serikali itafute namna ya kudhibiti jambo hili ili mkulima aweze kunufaika na kazi yake. Bw. Manjaule alieleza kuwa Ghala la Namitili limejengwa kwa fedha za Chama pamoja na mkopo wa Shilingi 30,000,000 waliopata kupitia benki ya CRDB na kufanya jumla ya fedha zilizotumika katika ujenzi huo ni shillingi 69,998,269.