Taasisi zinazohusika na maendeleo na usimamizi wa Sekta ya Ushirika nchini zimekubaliana kuimarisha Utekelezaji wa Mpango wa Mafunzo kwa Vyama Vya Ushirika wenye lengo la kuwajengea uwezo wanachama, viongozi na watendaji wa Vyama vya Ushirika.

Taasisi zilizokutana  Machi 23, 2022 Jijini Dodoma kwa lengo kufanya tathmini ya Utekelezaji wa Mpango huo ni Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO), Shirikisho la Vyama vya Ushirika nchini (TFC) na Muungano wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo Tanzania (SCCULT).

Akizungumza katika kikao hicho, Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, DKt. Benson Ndiege, amesema Kamati za Elimu na Mafunzo kwa Vyama vya Ushirika katika ngazi zote zinatakiwa kusimamia kikamilifu aina ya mafunzo yanayotolewa, wanaotoa mafunzo na wanufaika wa mafunzo hayo ili kupima ubora wake kwa Wanaushirika.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Profesa Alfred Sife, amesema kuwa Chuo hicho kimeweka msisitizo kwa Taasisi ya Elimu Endelevu na Ofisi za Mikoa kufanya tathmini ya ubora wa mafunzo yanayotolewa kwa Wanaushirika ili mafunzo hayo yaendane na mahitaji ya jamii husika.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO), Xavery Mkingule, amewataka watendaji kutoka katika Taasisi zinazohusika na maendeleo na usimamizi wa Sekta ya Ushirika nchini kushirikiana ili kuhakikisha kuwa Elimu ya Ushirika inayotolewa katika maeneo yao iwe inayokubalika na kuwanufaisha Wanaushirika.

Awali, akiwasilisha Utekelezaji wa Mpango huo wa Mafunzo, Dkt. Gervas Machimu kutoka Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo ambaye ni Katibu wa Kamati ya Elimu na Mafunzo kwa Vyama vya Ushirika kitaifa amesema katika kipindi cha kuanzia Machi 2021 mpaka Februari 2022, Chuo kupitia ofisi za mikoa kimetoa mafunzo kwa wanachama, viongozi na watendaji 8,415 (wanaume  5,812 na wanawake 2,603) wa Vyama vya Ushirika nchini.