Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa ametangaza uamuzi wa Serikali wa kuondoa tozo 42 kati ya 47 ambazo Wakulima wa Kahawa wa Mkoa wa Kagera walikuwa wanatozwa na kubaki tozo 5 ambazo zitakuwa na jumla ya Shilingi 267 kwa kila kilo ya Kahawa, kutoka Shilingi 830 za awali.

Waziri Mkuu ametoa maamuzi hayo kufuatia Tume maalum aliyoiunda ili kupitia utaratibu na Mfumo wa uendeshaji wa Vyama vya Ushirika wa zao la Kahawa Mkoani Kagera.

Mheshimiwa Majaliwa amewaagiza viongozi wa vyama vya Ushirika, wasimamie vyama vyao kwa uaminifu na weledi ili kuwaletea tija Wakulima wanaouza mazao yao kupitia Vyama vyao vya Ushirika.

Waziri Mkuu ametoa maelekezo hayo jana Jumanne, Machi 29, 2022 kwenye Kikao Maalum cha Wadau wa zao la Kahawa mkoani Kagera kilichofanyika wilayani Karagwe katika Mkoa wa Kagera.

"Tozo hizi zimekuwa nyingi mno na si tija kwa Mkulima ambaye sisi tunapaswa kumsimamia na kulisimamia zao hili kuepusha kutoroshwa na kuuzwa nchi za jirani," alisema Mhe. Majaliwa.

Tozo zitakazobaki ni Uendelezaji wa zao  la Kahawa  (Shilingi 100), AMCOS   (Shilingi 70), Union  (Shilingi 30), Halmashauri pamoja na vifungashio.

Vilevile, Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema kuanzia sasa mauzo ya Kahawa katika Mkoa wa Kagera yatafanyika kwa njia ya mnada ambapo minada hiyo itafanyika kwenye ngazi ya Vyama vya Msingi (AMCOS).