Kaimu Naibu Mrajis (Uratibu na Uhamasishaji) wa Vyama vya Ushirika, Consolata Kiluma amevitaka Vyama vya Ushirika vya mkoa wa Pwani kufuata taratibu na sheria za Ushirika ili kuufanya Ushirika kuwa wenye nguvu zaidi.

Naibu Mrajis ameyasema hayo leo tarehe 22/02/2023 mkoani Pwani katika Jukwaa la Ushirika lenye lengo la kufanya tathmini ya shughuli za Vyama vya Ushirika kila mwaka.

Aidha, Naibu Mrajis amevitaka Vyama vya Ushirika kuutangaza Ushirika ili  watu waelewe mafanikio na shughuli mbalimbali zinazofanywa na Ushirika.

"Nitoe wito kwenu watendaji wa Ushirika kuutangaza ushirika kupitia vyombo mbalimali vya Habari zikiwemo Televisheni, Redio, Magazeti,  na Mitandao ya Kijamii ili utambulike na wanaushirika, wananchi na Taifa kwa ujumla," amesema.

Naye Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika mkoa wa Pwani, Abdillah Mutabazi, amesema kuwa atahakikisha wanausimamia Ushirika kwa kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa na Ushirika ili kuwajengea wanaushirika na wasio wanaushirika kuwa na Imani na Ushirika.

Kwa upande wa Mkaguzi wa Vyama vya Ushirika  mkoa wa Pwani na Dar es salaam Brighton Mwang'onda amesema kuwa ili kuondokana na Hati Chafu, watendaji wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanakuwa na taarifa sahihi za kifedha.