Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Dkt. Benson Ndiege, amewataka Warajis Wasaidizi wa Vyama vya Ushirika wa Mikoa kuhakikisha kuwa katika maeneo yao kunakuwa na udhibiti wa migogoro katika Vyama vya Ushirika.

“Msisubiri migogoro iwe mikubwa katika Vyama, kwa kuwa inaharibu taswira ya Sekta ya Ushirika, hakikisheni mnashughulikia migogoro hiyo inapojitokeza na kutoa suluhisho; migogoro itakayofikishwa ngazi ya Taifa inaonyesha udhaifu wa uongozi katika eneo husika,” amesema Dkt. Ndiege.

Mrajis ameyasema hayo katika Kikao cha siku mbili na Warajis Wasaidizi wa Vyama vya Ushirika wa Mikoa, kilichofanyika Jijini Dodoma kuanzia tarehe 24 – 25 Machi, 2022 ambapo amewataka kushughulikia migogoro inayojitokeza kwa kuzingatia Sheria ya Vyama vya Ushirika Na. 6 ya Mwaka 2013 na amesisitiza umuhimu wa kushirikiana na Wanasheria waliopo katika Ofisi za Mikoa katika kutatua migogoro inayojitokeza.

Aidha, Mrajis wa Vyama vya Ushirika amewataka Warajis Wasaidizi wa Vyama vya Ushirika wa Mikoa kuwa na Ushirikiano na Taasisi na Mamlaka nyingine zilizoko katika maeneo yao na kutoa ufafanuzi kuhusu Maendeleo na uendeshaji wa Ushirika ili kuwa na uelewa wa Pamoja katika utekelezaji.

“Shirikianeni na kutoa taarifa za Utekelezaji  na Mafanikio ya Sekta ya Ushirika kwa Taasisi na Mamlaka zilizoko katika maeneo yenu ili kufanikisha malengo ya Taifa katika kuimarisha Sekta ya Ushirika na kuinua Uchumi wa Wananchi kwa ujumla,” amesema Mrajis.