Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mheshimiwa Adam Malima   ametoa wito kwa Wanaushirika wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo kuwekeza kwenye Uchumi wa Viwanda ili kukuza hali ya Viwanda Nchini.

Ameeleza hayo wakati anafunga Maadhimisho ya 74 ya siku ya Kimataifa ya Ushirika wa Akiba na Mikopo kwa mwaka wa 2022 yaliyokuwa yakifanyika Jijini Mwanza katika Viwanja vya Furahisha, yenye kauli mbiu: 'Imarisha uwezo wako wa kifedha kwa siku zijazo kupitia ushirika wa akiba na mikopo'.

Mheshimiwa Malima amesema kuna SACCOS zina uwezo mkubwa ambazo zikiamua kuwekeza katika suala la viwanda kwao ni jambo dogo na ambalo linaweza kufanikiwa kama wakiamua kwa moyo mmoja na wakiaminiana.

"Mnaweza kuwekeza katika viwanda tukaongeza kukuza uchumi wa viwanda Tanzania tena ikiwezekana unganeni nyie SACCOS zenye mafanikio ili muoneshe mfano kwa hawa wengine," amesema Mhe. Malima.

Pia amevitaka Vyama vya Ushirika kuendelea kununua Hisa katika Benki ya Ushirika Kilimanjaro (KCBL) ili kuifanya kuwa na nguvu zaidi na kuiomba Serikali kuweza kununua hisa pia katika benki hiyo ambapo kiasi cha shilingi bilioni 15 zinahitajika katika kuifanya kuwa benki ya Ushirika.

"Unajua zamani ulikuwa ukisikia ushirika unasema hamna kitu pale ila sasa hivi ukisikia ushirika unashituka maana ushirika ya sasa inafanya mambo makubwa hata mie nimenunua hisa na watu wengine pia nunueni hisa katika Benki ya Ushirika," amesema Mhe. Malima.

Naye Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Akiba na Mikopo Tanzania Bara, (SCCULT 1992 LTD), Eng. Dkt Cuthbert Msuya, amesema SACCOS zimechangia katika kuboresha maisha ya jamii kwa kuwawezesha wanachama, kupata mitaji, kugharamia elimu kwa watoto wao, kumudu gharama za afya, kumiliki vyombo vya usafiri na vifaa mbalimbali pamoja na makazi bora.

Wakati huo huo Mrajisi wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege, amesema bado kuna changamoto katika utoaji wa taarifa za ukaguzi kutokana na kutokuwepo usimamizi makini wa mali za ushirika.

"Mie nalia na Mameneja wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo kutokana na hizi Hati Chafu mnazopata; ukijiona una miaka miwili unapata Hati Chafu jua wewe hautoshi ulipo, jiengue mapema maana tutakuchukulia hatua kwa kushindwa kukisimania chama chako," amesema Mrajis.

MWISHO