Kamisheni ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) imeanza kutekeleza mpango wa kubadili namna ya kuendesha Vyama vya Ushirika na kuviwezesha kutumia Teknolojia za kisasa katika kufanya shughuli zao.

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Abdulmajid Nsekela, ametoa taarifa hiyo leo tarehe 27/02/2023 wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Wadau wa Ushirika Jijini Dar es Salaam, unaolenga kujadili maendeleo ya Ushirika na kuweka mkakati wa kuimarisha Sekta hiyo hapa  Nchini.

Nsekela amesema, Uwekezaji katika mifumo ya kisasa ya kidijitali utaongeza ufanisi wa kiutendaji katika Vyama vya Ushirika, pamoja na Mamlaka za Usimamizi wa Sekta hiyo.

Ameongeza kuwa, pamoja na mambo mengine mapendekezo yatakayotolewa katika mkutano huo yatasaidia kuboresha Mfumo wa Ushirika na kuufanya wa kisasa zaidi na kuwawezesha wananchi kushiriki ipasavyo kwa ustawi wao na wa Taifa kwa ujumla.

“Ni matumaini yangu kuwa Maazimio yatakayofikiwa kupitia mkutano huu yatapaswa kutekelezwa ipasavyo na kila mdau na kwamba taarifa ya utekelezaji itakuwa inatolewa na kujadiliwa mara kwa mara,”amesema Nsekela.

Kwa upande wake Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Dkt. Benson Ndiege, amesema lengo kubwa la mkutano huo wa Wadau wa Ushirika ni kujadili maendeleo ya Ushirika na kuweka Mkakati wa kuimarisha Sekta hiyo hapa nchini.  

“Mkutano huu ni muhimu kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo ya Ushirika hapa nchini, lakini pia tumekutana wadau wote ili kuja na mapendekezo ya pamoja ya kuendeleza Sekta hii kwa maendeleo ya Taifa,” ameongeza Mrajis.

Aidha, Dkt. Ndiege amesema, kila aliyepewa dhamana atekeleze majukumu yake ili kuujenga Ushirika ulio imara ambao utawasaidia wananchi katika kuboresha uchumi wao.

“Tushirikiane kuujenga Ushirika nafurahi sasa hivi kuona Vyama Vikuu vya Ushirika vinasaidia katika kutoa misaada katika huduma za kijamii, endeleeni kurudisha mnachokipata kwa jamii,” amesema Dkt. Ndiege.