Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MOCU), Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO), Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) na Chama Kikuu cha Ushirika wa Akiba na Mikopo (SCCULT) wamesaini Mpango wa Mafunzo ya Wanachama Viongozi na Watendaji wa Vyama vya  Ushirika, Tanzania Bara. Mpango huu unatekelezwa na Taasisi hizo na ni wa muda wa mwaka mmoja.

Mpango huo umesainiwa leo tarehe 20/10/2022 katika kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya 74 ya Ushirika wa Akiba na Mikopo Jijini Mwanza. Mwakilishi wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika (MOCU) Dkt Grevas Machimu, amesema lengo la mpango huu ni kutoa mafunzo yatakayowezesha uimarishaji wa uendeshaji na usimamizi wa vyama vya ushirika ili kutoa huduma kwa tija na kukidhi mahitaji ya wanachama kiuchumi na kijamii.

Alisema kuwa anatarajia  mafunzo kupitia mpango huu wanaushirika kuongeza tija katika kazi zao kwani watakuwa washapata mafunzo ambayo yanawajenga katika utendaji kazi wao wa kila siku.

Dkt. Benson Ndiege Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirikia Tanzania amewaagiza Warajis Wasaidizi wa Mikoa kusimamia mpango huo na kuhakikisha kila chama kinapata mafunzo.

"Sisi ni Serikali hatufanyi biashara, tunatoa huduma hivyo gharama ziendane na uhalisia tusifanye biashara ili kila mwanaushirika anufaike na mpango huu," amesema Dkt. Ndiege.

Vile vile amesema Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi kimekuwa na programu fupi fupi za mafunzo ambayo wanaushirika wanazipata ila kumekuwa hakuna mpango wa kufuatilia kama wanufaika wa mafunzo hayo wamefanikiwa kwa mafunzo au bado wana changamoto.

"Hatuna mpango mzuri wa kupima watu wetu wakipata mafunzo ni muhimu kujua kama mafunzo mnayotoa yanakuwa na tija na yamevisaidiaje vyama, ili kujua tunachotoa kina manufaa kwa wanaushirika au hakina," amesema Dkt. Ndiege