Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. David  Kafulila, amesema Serikali ya Awamu ya sita chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan, imetenga kiasi cha Shilingi Billion sita (6) kwa ajili ya kufufua Viwanda vya Pamba Mkoani Simiyu.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu amesema kuwa kufufuliwa kwa viwanda vya Pamba vinavyomilikiwa na Ushirika kutapelekea  kufanya vizuri kwa zao la Pamba katika Ushirika kwa msimu huu baada ya kuzitatua changamoto zote zilizokuwa zinakwamisha zao hili.

Mheshimiwa Kafulia ameyasema hayo katika Mkutano Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoani Simiyu (SIMCU)

uliofanyika  jana tarehe 05/04/ 2022, Mjini Bariadi.

"Sisi tunaongoza kwa Pamba hapa Tanzania, Vyama vyetu vya Ushirika vikijisimamia kuanzia ngazi ya msingi na vijiji vitaimarika kutokana na usimamizi wa mauzo ya Pamba kupitia Mfumo wa Ushirika," amesema Kafulila.

Akizungumza katika Mkutano huo, Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, ametaka uongozi mpya utaochaguliwa kwenda kusimamia maslahi ya wakulima wa zao la Pamba kuepuka tuhuma mbalimbali zinazoelekezwa kwa baadhi ya Viongozi wa Vyama vya Ushirika kutokuwa waadilifu.

Aidha, Mrajis ameshauri kuwa watendaji katika ngazi ya Karani Wahasibu kuajiriwa wanaotoka ndani ya mkoa husika kuepuka Chama kuibiwa na kukimbiwa mara kwa mara.

 Mkutano Mkuu wa SIMCU  uliambatana na uchaguzi wa Viongozi wa Bodi mpya ya Chama Kikuu cha Ushirika SIMCU, baada ya Bodi iliyokuwa madarakani kumaliza muda wake.

Viongozi wapya wa Bodi ya SIMCU waliochaguliwa ni Mwenyekiti, Lazaro Walwa, Makamu Mwenyekiti, Kulwa Bupuna na Wajumbe ni Makoye Bwile, Philimon Sambe, Susan Masanja, Simon Magoma na Shiboka Petro. Mwakilishi ni Jenipha Emanuel.